Monday, 29 October 2007

Tanzania yaombwa kuandaa fainal za afrika 2009


TANZANIA imeombwa na Baraza la Vyama vya Mpira wa Miguu Afrika Mashariki na Kati (CECAFA), kuwa mwenyeji wa mashindano ya nchi bingwa wa Kanda za Afrika II yanayotarajia kufanyika kwa mara ya kwanza mwaka 2009. Mashindano hayo ambayo ni mara ya kwanza kufanyika katika Afrika, yatashirikisha timu nane, ambazo ni bingwa kutoka kila kanda kwa Afrika na yatashirikisha wachezaji wanaocheza soka ndani ya nchi tu. Akizungumza jana Dar es Salaam, Katibu Mkuu wa CECAFA, Nicholaus Musonye, alisema wameipendekeza Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano hayo, kutokana na changamoto ya nchi hiyo katika kukuza soka na maendeleo ya viwanja vya soka waliyokuwa nayo. Alisema kesho CECAFA itakutana na uongozi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), pamoja na Serikali kuzungumza ombi la CECAFA kuichagua Tanzania kuandaa mashindano hayo, ambapo anatarajia ombi hilo litakubaliwa kutokana na faida inayopata nchi mwenyeji na manufaa yake kwa Taifa. "Lengo la kuichagua Tanzania kuwa waandaaji wa mashindano haya ni kutokana na kuthamini mchango wao katika kukuza soka, pia Tanzania kwa sasa inaongoza katika Afrika Mashariki na Kati kuwa na viwanja vizuri vyenye ngazi ya kimataifa," alisema Musonye. Alisema lengo la CECAFA kutaka kuwa mwenyeji wa mashindano haya ni kutaka kupata nafasi mbili za kushiriki, ambapo kanda itakayoandaa mashindano inapata nafasi mbili, ambapo nafasi moja ni timu mwenyeji na nyingin ni bingwa husika na mashindano hayo yamepangwa kufanyika mwaka 2009. Alisema CECAFA inamaliza mazungumzo ya mwisho na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), ili kupata na wana matumaini makubwa ya kuipata nafasi hiyo kwani ndiyo kanda pekee kwa Afrika inayoandaa mashindano mara kwa mara. Wakati huo huo, CECAFA imesema mashindano ya Chalenji kwa wanaume yatafanyika Dar es Salaam, kuanzia Desemba 8 hadi Desemba 22, mwaka huu na timu zote tayari zimthibitisha kushiriki. Alizitaja nchi zilizothibitisha kuwa ni Tanzania,Kenya, Uganda, Somalia, Rwanda, Burundi, Elitrea, Sudani, Jibuti, Zanzibar na Ethiopia.

No comments: